Kufundisha kwa ajili ya Kesho: Namna Grumeti Fund inavyosaidia kwenye Elimu katika Jamii

Mpango wa Msaada wa Ufundishaji wa Grumeti Fund unalenga kuimarisha elimu kwa wanafunzi wa shule ya msingi katika vijiji 22 vinavyopakana na mapori ya akiba ya Ikorongo – Grumeti. Mpango huu ulizinduliwa na kuanza rasmi mwezi Februari mwaka 2021. Mpango wa Msaada wa Ufundishaji huwapeleka walimu vijana na wenye ari katika shule za msingi 26 tofauti zinazopakana na mapori haya ya akiba. Mwaka huu jumla ya walimu 50 watakuwa na majukumu ya kufundisha Sayansi, Hisabati, na Kiingereza katika shule zinazokabiliwa na uhaba wa walimu katika vijiji hivi. Walimu hawa wanajenga msingi wa kitaaluma wa wanafunzi, kuwawezesha kufanikiwa katika juhudi zao za kitaaluma za baadaye.

Zaidi ya walimu hawa kukabiliana na majukumu makubwa darasani, pia wamejizatiti kuongeza ari na ushiriki wa wanafunzi wao shuleni kwa ujumla. Kwa kutumia mbinu bunifu za kufundishia, wanajumuisha ufundishaji darasani na ngoma za asili, nyimbo, na maigizo ili kufanya kujifunza kuwa kwa kusisimua na wenye ufanisi zaidi. Walimu hawa pia wanatumia shughuli za ziada nje ya mtaala wa elimu ili kujenga ujasiri wa wanafunzi, kuchochea shauku zao, na kuwaweka karibu na jamii yao ya kitaaluma.

Picha: Kulia ni Fides Gau, Kocha wa programu hii ya msaada wa ufundishaji akiwa katika moja ya vipindi darasani na miongoni mwa walimu hao.

Katika mazungumzo na Fides Gau, kocha wa Mpango wa Msaada wa Ufundishaji, kwanza alishiriki kauli mbiu ya mpango huo, “Upendo kabla ya kufundisha.” Ilionekana wazi kwamba neno hili rahisi lilikuwa zaidi ya maneno tu kwenye ukurasa, bali ilikuwa nguvu inayoendesha kila kitu ambacho walimu wa Msaada wa Ufundishaji wanafanya.

Fides amekuwa kocha tangu mwanzo wa programu hii mwaka 2021, na alielezea, “Mpango huu umebuniwa mahususi kushughulikia changamoto ya uhaba wa walimu katika maeneo ya vijijini, hasa katika vijiji vinavyopakana na mapori haya ya akiba. Tunatambua kuwa kila mwanafunzi anastahili kupata elimu bora, bila kujali hali yake kiuchumi. Na ndiyo hasa tunacholenga kutoa kupitia programu hii.”

Mpango huu unalenga kuwajengea wanafunzi wa shule ya msingi zaidi ya maarifa ya kitaaluma pekee, bali pia stadi muhimu za maisha na maadili kama vile heshima, ushirikiano, na uwajibikaji. Kwa kufanya hivyo, walimu walio kwenye programu hii wanaimarisha malengo makuu ya mpango – kuchochea upendo wa kujifunza na kuhamasisha watoto kufikiri kwa ubunifu na kwa kina.

Picha: wanafunzi wakiwa katika moja ya michezo baada ya vipindi darasani.

Fides alisisitiza, “Timu yetu ya walimu wenye uzoefu inashirikiana kwa karibu na shule za maeneo haya ili kubuni na kutekeleza shughuli za kujifunza za kufurahisha na shirikishi ambazo zinakidhi mahitaji tofauti na mitindo ya kujifunza ya kila mtoto.”

Fides aliendelea kueleza kwamba katika jamii hizi, watoto wengi wanatoka katika familia zenye kipato cha chini na wanaweza kuwa na mahitaji ya kitaaluma na kihisia ambayo hayajakidhiwa. Hata hivyo, kupitia Programu ya Usaidizi wa Ufundishaji, walimu hawa hutoa nafasi kwa wanafunzi kuonekana, kusikilizwa, na kupewa malezi ya kiakili na kimwili. Walimu walio kwenye mpango huu wanatambua uwezo wa kila mtoto na huchukua muda wa kumsikiliza na kuungana na kila mmoja, wakitoa msaada wa kisaikolojia ambao yamkini wanaweza kukosa.

Grumeti Fund tunaamini kuwekeza katika elimu ya wanafunzi wadogo ni muhimu katika kujenga viongozi na wahifadhi wa baadaye ambao wataendeleza maendeleo yenye manufaa kwenye mazingira na kwa wanyama pori ili kulinda sayari yetu. Kwa kusaidia Programu yetu ya Msaada wa Ufundishaji, sio tu unatoa elimu bora kwa watoto wadogo – pia unawekeza katika mustakabali wa mazingira yetu.

Jiunge nasi katika safari hii ya kusisimua inayochochoe kizazi kijacho cha wahifadhi na viongozi waadilifu na wenye kuwajibika.

Kuchangia programu hii, bofya hapa

                  

Tafadhali tambua kuwa unahamishwa kwenda kwenye kurasa ya Shirika la Uhifadhi na Jamii za Kiafrika, Inc.

Nchini Marekani, Grumeti Fund ni mradi unaosaidiwa-kifedha na Shirika la Uhifadhi na jamii za Kiafrika, Inc. (“ACCF”), shirika la kimsaada 501(c) (3). Michango yenye kutozwa kodi kwa ACCF hutolowa kwa Grumeti Fund kusaidia kazi yetu.

Bonyeza hapa kuchangia