Ng’ombe kwa Uhifadhi
Vipi kama Ng’ombe wa maziwa huweza kubadilisha maisha? Hiki ndicho kinachotokea kwenye vijiji 21 vinavyopakana na mapori yetu ya akiba ya Ikorongo – Grumeti. Kupitia mradi wetu wa ng’ombe bora wa maziwa ulioko chini ya programu ya Climate-Resilience and Improvement Program (CLIP) sio tu tunalinda wanyamapori bali pia tunabadilisha maisha ya jamii za wenyeji.
Uhifadhi endelevu ni zaidi ya kulinda maliasili – ni kuboresha jamii za pembezoni na maeneo ya uhifadhi na kuishi kwa amani baina ya binadamu na wanyamapori. Mtazamo huu ulitusukuma kuanzisha mradi wa ng’ombe bora wa maziwa mwaka jana ili kuwainua wajasirimali. Tulianza na wajasiriamali 15, miongoni mwao wanawake wanne.
Leo hii wajasiriamali hawa wameanza kuona matunda ya mradi huu. Ng’ombe sita kati ya kumi na tano waliotolewa wameishazaa, hivyo kuwapatia wanakijiji hawa maziwa kama chakula kwa kujipatia protini nyumbani na kuuza kama sehemu ya kujiingizia kipato. Kila ng’ombe hutoa angalau lita 15 kila siku sawa jumla ya lita 105 kwa wiki. Huu ni uhakika wa maziwa yenye lishe kwa ajili ya familia hizi na mapato. Katika jamii ambazo usawa kati ya wanawake na wanaume ni mdogo, mradi huu umeleta mabadiliko na kuongeza uhuru wa kifedha na kuimarisha familia.
Kuendelea na mchango huu mkubwa, wajasiriamali wengine 15 waliochaguliwa kwa uangalifu walipatiwa ng’ombe wa maziwa wajawazito (kati ya miezi 5 hadi 8). Wajasiriamali hawa wamefundishwa sio tu namna ya kuwatunza ng’ombe hawa lakini pia uzalishaji wa malisho na njia za kuwahudumia ng’ombe kama vile kuwachoma chanjo za muhimu. Kwa kuwafundisha na kuwapatia rasilimali zinazohitajika kwa ufugaji wa kisasa wa ng’ombe wa maziwa tunaimarisha uchumi endelevu kwa familia hizi na kupunguza shughuli za uharibifu wa mazingira kama vile biashara haramu ya nyamapori na ukataji miti kwa ajili ya uchomaji wa mkaa.
Programu hii ya CLIP huenda zaidi ya kuboresha maisha – ni mradi wa kuwezesha jamii hizi kwa vizazi vingi vijavyo. Bageni George, miongoni mwa wanawake saba walionufaika na awamu ya pili ya mradi huu wa ng’ombe wa maziwa. Anasema:
“Ng’ombe huyu ni ishara ya mabadiliko ya mitazamo, mila na desturi za muda mrefu kwenye jamii zetu na kumwezesha mwanawake. Kama mama wa watoto wanne na bibi wa wajukuu watano hii ni baraka itakayo boresha maisha yetu. Ng’ombe huyu ataimarisha kipato changu na kuwa chanzo thabiti cha maziwa yenye lishe kwa familia yangu. Kufahamu kuwa familia yangu watakuwa na afya nzuri na uhakika wa kipato kunanifanya niwe mwenye shukrani, furaha na matumaini”
Bageni George akiwa na ng’ombe wake aliyepewa.
Mradi huu utaleta matokeo endelevu nay a muda mrefu kwa kuunganisha uhifadhi na uwezeshaji wa jamii.
“Ndani ya miaka 5 hadi 10 ijayo mradi huu utaboresha mazingira ya maeneo ya jamii kwa kupunguza shinikizo la malisho na kuzuia uvamizi wa ng’ombe kwenye maeneo ya hifadhi. Kuimarisha uhusiano wa soko na mnyororo wa thamani uliowekwa vizuri itakuwa muhimili muhimu kwa mafanikio na uendelevu wa mradi huu.” – Frida Mollel, Mkuu wa Idara ya Ufikiaji wa Jamii
Ungana nasi kwenye kutengeneza ubadaye ambapo binadamu na Wanyama hustawi pamoja kwa amani. Bofya hapa kuunga mkono kazi yetu na kuwa sehemu ya mabadiliko.