Kukabiliana na Mimea Vamizi.
Fikiria ikolojia nzuri iliojaa mimea, mamia ya aina za ndege na wanyamapori wanaostawi katika makazi yao ya asili. Ni tukio la kupendeza ambalo sote tunatumai kuhifadhi kwa vizazi vijavyo. Lakini vipi nikikuambia mahali hapo panakabiliwa na tishio la spishi vamizi?
Mapori ya akiba ya Ikorongo – Grumeti yaliyoko Magharibi mwa Serengeti, ambayo hapo awali yalikuwa katika hali mbaya ya kutokuwa na wanyama, na sasa ni mfumo wa Ikolojia unaonawiri, yako kwenye tishio la spishi za mimea vamizi.
Baraka Kereto, anaefanya kazi Grumeti Fund kama meneja wa kanda, ambapo anajishughulisha na kupambana na kutokomeza spishi za mimea vamizi kwa kiasi kikubwa.
Grumeti Fund ilianza kazi ya kudhibiti na kutokomeza spishi ngeni vamizi (IAS) mwaka 2009, kufuatia uchunguzi uliobainisha spishi za mimea vamizi sita hatari zaidi kwenye mapori hayo, ambayo ni: Opuntia spp, Chromolaena odorata, Lantana camara, Pistia stratiotes, Parthenium hysterophorus, na Tithonia diversifolia.
Baraka na timu yake hutumia njia za kutumia nguvu na kemikali kudhibiti na kuangamiza mimea hii. Wanang’oa na kuikata mimea na kisha kuinyunyizia dawa za kuua magugu. Mara nyingi njia inayotumiwa inategemea hatua ya ukuaji wa mmea.
Kuna timu mbili ambazo zinahusika katika kutokomeza spishi za mimea vamizi. Kila timu huwa na watu kumi na sita wakati wa kiangazi na watu tisa wakati wa msimu wa mvua. Kwa ufanisi washiriki wa timu katika zoezi hili hufunzwa jinsi ya kutumia vifaa na zana mbalimbali pamoja na umuhimu wa kufanya kazi kwa karibu kama timu. Kufanya kazi kama timu ni muhimu, si tu kwa umahiri na ufanisi lakini pia kwa usalama.
Siku ya kawaida kwa mshiriki wa timu huanza kwa kuamka saa kumi na moja asubuhi, kuendesha gari hadi eneo zilipo spishi za mimea vamizi, na kugawanya eneo katika miraba kwa ufanisi. Siku ya kazi kawaida ni masaa nane na wakati mwingi wanafanya kazi kwenye eneo la ukubwa wa mita za mraba 10,000.
“Mfumo wa ikolojia utaharibika ikiwa spishi ngeni vamizi hazitadhibitiwa. Niche ya kiikolojia ni sehemu ya kwanza ya makazi asilia kuathiriwa na spishi ngeni vamizi; hili likishafanyika vipengele vingine kama vile lishe, kuzaliana, ukuaji wa wanyama na mimea vitaathirika. Hatimaye mazingira na makao ya asili yanapoharibiwa, baadhi ya wanyama, wadudu, na mimea wanaweza kutoweka na hivyo kuhatarisha si uwepo wao tu bali pia uwepo wa wanadamu.” Alisema Baraka.
Baraka na timu yake wanafanya kazi bila kuchoka kudhibiti na kutokomeza spishi hizi vamizi. Ana imani kwamba kwa msaada wa wadau wakuu wa uhifadhi, jamii, na serikali tatizo hili linaweza kupungua kwa kiasi kikubwa.